Karibu DSN TECHNOLOGY – Sehemu Pekee Unayoweza Kujifunza Teknolojia Bila Kuchoka
Sasa Hebu Tukubaliane Hivi...
Unayo bidhaa nzuri kama maandazi ya asubuhi au huduma kali kama msemo wa mama yako, ila bado haujaweka biashara yako Facebook? Hii ni sawa na kuwa na mgahawa unaopika chipsi mayai tamu, lakini huna kibanda – unazipikia porini!
Leo hapa DSN TECHNOLOGY, nakupa mwongozo wa namna ya kutengeneza Facebook Page ya kibiashara, hatua kwa hatua, bila maneno mengi ya kichina au misamiati ya "techie" inayoonekana kama imetoka kwenye Mars. Huu ni mwongozo wa mtu wa kawaida, aliye na simu, internet, na ndoto ya kufanikiwa.
Kwanza Kabisa: Kwanini Utengeneze Facebook Page?
Acha nikuambie kitu kimoja cha ukweli – watu hawakai tena barazani, wako kwenye mitandao. Na Facebook ni kama 'soko kuu la Kariakoo' la mtandaoni – kila mtu yupo pale, anachek bidhaa, anatafuta huduma, na pia... anapiga like kwa picha za mbwa wa watu.
Faida kuu za kuwa na Page ya biashara:
- Wateja wanakupata kirahisi
- Unatangaza bure (na ukitaka, kwa hela kidogo unalipua)
- Unaaminika zaidi (kuliko kusema "niko Instagram tu")
- Unaweza kupokea oda, kutoa taarifa, na hata kuendesha kampeni zako pale pale
Sasa Twende Kazi: Hatua kwa Hatua za Kutengeneza Page
1. Fungua Facebook kwenye simu au kompyuta yako
Kama bado huja-log in, ingia kwanza. Usiwe yule mtu ambaye anasahau password kila baada ya siku tatu – Facebook haina uvumilivu huo!
2. Nenda kwenye Menu > Pages > Create
Ukishafika hapo, bonyeza 'Create New Page'. Hapo ndipo kila kitu kinapoanzia.
3. Andika Jina la Biashara Yako
Hakikisha jina linaeleweka. Kama unauza vitenge, usiandike jina la "Sweetheart Empire" halafu mtu ajue unauza maua. Mfano mzuri: "Vitenge Vyetu by Rehema" au "Mambo Poa Electronics"
4. Chagua Category
Hii ni muhimu kuliko vile unavyofikiria. Chagua aina ya biashara yako. Kama unauza nguo, andika "Clothing Store". Kama unatoa huduma, andika "Service".
5. Maelezo Mafupi (Description)
Hapa andika kwa kifupi biashara yako inahusu nini. Mfano: "Tunauza vitenge vya kisasa kutoka Kitenge Street, Dar. Urembo wa kiafrika, bei za kinyumbani."
6. Picha ya Profile na Cover
Tumia picha inayowakilisha biashara yako. Kama unauza chakula, weka picha halisi ya chakula (sio ile ya Google). Cover image iwe ya duka au bidhaa zako.
7. Bonyeza 'Create Page' – BOOOM! Umemaliza.
Bada ya Hapo? Hii Ndio Siri ya Mafanikio:
- Weka Post Mara kwa Mara: Usiwe na ukurasa kama kaburi – kimyaaa! Weka picha, ofa, status, hata story za wateja.
- Jibu Comments na Inbox Haraka: Ukichelewa, mtu anahamia kwa mshindani. Uliza tu wenye duka Kariakoo.
- Tumia WhatsApp Link: Unganisha WhatsApp yako ili wateja wakugonge tu – unapata oda papo hapo!
- Boost Post kwa Tsh 2,000: Ukitaka wateja wengi, boost tangazo moja moja. Unaweza kulenga watu wa Arusha tu au wanaopenda viatu.
Bonus: Epuka Makosa Haya
- Usijaze emoji za kila aina hadi ukurasa uonekane kama chapisho la mtoto wa darasa la tatu.
- Usitukane wateja hadharani – hata kama wamekuudhi kama wifi.
- Usitumie picha za watu wengine – weka zako. Wateja si wajinga.
SASA ACHA TUKWAMBIE...
Kutengeneza Facebook Page ni hatua ndogo sana, ila matokeo yake yanaweza kuwa makubwa kuliko foleni ya CRDB mwisho wa mwezi. Anza sasa – hata kama huna bidhaa nyingi. Muhimu ni kuanza. Biashara nzuri hujengwa kwa juhudi na mwonekano.
Na kama umefaidika na post hii, si vibaya uka-share kwa mtu mmoja tu. Unajua wema hulipwa – lakini si lazima kulipwa na mpesa, hata share moja ni baraka.